Tanzania itatoa tani 500 za chakula kwa Serikali ya Sudan Kusini ikiwa ni msaada wa kuwasaidia wananchi walioathiriwa na vita katika baadhi ya majimbo nchini humo.
Mbali na msaada huo pia Serikali ya Sudan Kusini imeiomba Tanzania kusaidia kujenga uwezo katika vyama vya ushirika, kufanya utafiti na mafunzo kwa maafisa ugani kwa kuendesha mafunzo ya kilimo katika vyuo vyake vya kilimo, kuanzia ngazi ya cheti hadi Shahada.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, alisema hayo mwishoni mwa wiki katika ziara ya siku mbili nchini Sudan Kusini, ambako alikutana na Makamu wa Rais wanchi hiyo, Jenerali James Wani Igga, mjini Juba.
Chiza alisema Tanzania ipo tayari kushirikiana na Sudan Kusini kuimarisha sekta ya kilimo, kuanzia kwenye uzalishaji, masoko, ikiwa pamoja na kuwawezesha wakulima kutumia zana bora za kilimo.