Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf ametangaza amri
ya kutotoka nje nyakati za usiku kuanzia saa tatu hadi saa kum na mbili
asubuhi.
Watu hawataruhusiwa kuingia au kutoka nje ya eneo la kitongoji cha West Point viungani mwa jiji la Monrovia.Aidha, eneo fulani katika mji mkuu wa Monrovia litatengwa katika harakati za kuthibiti kuenea kwa ugonjwa hatari wa Ebola.
Watu waliojawa na hamaki walishambulia kituo cha afya katika eneo la West Point siku ya Jumamosi, na kupelekea kutoroka kwa wagonjwa 17 wa Ebola.
Rais Sirleaf amelaumu serikali yake kwa kutothibiti homa hiyo ya Ebola, kwani haikufanya vya kutosha kuboresha hali ya maisha ya raia walipopuuza ushauri wa wafanyakazi wa huduma za afya na kutotilia maanani tahadhari rasmi za Ebola.
Hata baada ya Liberia kutangaza hali ya dharura kufuatia mlipuko wa Ebola mapema mwezi huu, ugonjwa huo unazidi kusababisha vifo nchini humo.
Ebola haina tiba lakini Shirika la Afya Duniani (WHO) liliidhinisha matumizi ya dawa zilizokuwa zikifanyiwa utafiti kufuatia mlipuko mkubwa wa Ebola Afrika Magharibi
Kwa mujibu wa waziri wa maswala ya habari wa Liberia, Lewis Brown, madaktari watatu walioambukizwa Ebola wakiwahudumia wagonjwa wa Ebola, wameonyesha dalili za kuimarika kiafya, baada ya kutumia dawa zilizokuwa zikifanyiwa majaribio juma lililopita.
Watu 1,229 wameripotiwa kufarika katika kanda ya Magharibi mwa Afrika tangu ugonjwa huo uzuke miezi minne iliyopita.
Ebola husambazwa moja kwa moja kupitia maji maji ya mwili ya waliougua