Wapiganaji wa mashariki mwa Ukraine wanaoipendelea Urusi wamewaendesha kwata katika barabara za mji wa Donetsk, wanajeshi kadha wa Ukraine waliowateka.
Donetsk ni ngome ya wapiganaji hao.
Mambo hayo yamejiri siku ya kuadhimisha uhuru wa Ukraine.Watu waliosimama kando ya barabara waliwazomea "mafashisti" wafungwa hao walioonekana wachafu.
Katika kuadhimisha siku hiyo Rais wa Ukraine, Petro Poroshenko, aliahidi kutumia dola bilioni 3 kulipatia jeshi zana mpya katika miaka mitatu ijayo.
Akitoa hotuba kwenye gwaride katika mji mkuu, Kiev, Rais Poroshenko alisema Ukraine imekuwa ikipigana vita hasa dhidi ya uvamizi wa kigeni, na Ukraine itakabili tishio la kijeshi kila mara katika siku za usoni:
"Kufuatana na mpango wa mwaka 2015-17 dola bilioni 3 zitatumiwa kununua silaha na zana mpya za kijeshi.
Hiyo itawezesha kukarabati, kununua na kulipatia jeshi ndege, helikopta, manuwari na mashua.
Huu ndio mwanzo tu."